Riwaya
Msomaji wa Blog yangu ya Auntrahmaonlinetz, nilitoa sehemu ya kwanza ya riwaya na kuiacha kwa muda kutokana na majukumu. Sasa nairejesha na kuunganisha sehemu ya pili ya hadithi Safari ya Tanga. Ni riwaya yenye kuburudisha na kuelimisha
Safari ya Tanga
Nimepewa barua ya kikazi kwenda mkoani Tanga kwa muda wa miezi
sita, baada meneja aliyekuwepo hapo,
kupata matatizo ya Kiafya. Mji ulikuwa mgeni kwangu. Familia yangu, ikiwemo mke
na watoto niliwaacha jijini Dar es salaam.
Mke wangu hakusita kuniusia juu ya jiji la Tanga lenye Wanawake
warembo na lugha laini. Alinionya sana mchepuko wa Tanga siyo dili. Ukijaribu
unazama moja kwa moja na kusahau familia yako.
Alinieleza maji ya kuoga utawekewa hiliki na asmini kitandani hapo
unaweza kujisahau.Utaimbiwa taarabu nyepesi za Bi Shakira na kuingia mtegoni.Huku
udi ukinukia chumba kizima mbali na mwanandani mwenyewe, aliyejiosha kwa maji
ya Waridi.
Niliapa nitaenda kwa kile
kilichonipeleka na si kingine.Nilifuata moja huko, sikubali kumi na moja. Mtoto
wa bara miye mambo hayo kwangu siyo!.
Mh!. Kuanzia kazini mpaka nyumbani ilikuwa mitego mitupu. Hatimaye
nikajikuta pendo linazama kwa binti aliyekuwa katibu muhktasi wetu pale
ofisini. Haikuwa kazi rahisi kumpata kama nilivyoelezwa.
Mtoto wa Kisegeju alikuwa hategeki. Alijiwekea msimamo thabiti.
Hapo nikaamini kwamba si Wanawake wa kitanga wepesi kila mwanadamu na hulka
yake.
Alinichanganya vilivyo mtoto Waseme. Aingiapo kazini, utasikia
harufu nzuri ya uturi kuanzia mlangoni. Hapo akili zote zilihama. Usia wa mama
watoto nikatupia kule!.
Binti huyu Waseme alinitoa jasho!.Ilinibidi nitumie nguvu za
ziada kuwa karibu na mimi.
Tayari alishaingia katika kumi na nane zangu. Nilimficha kwamba
sijaoa. Binti wa kitanga niliapa kutomkosa. Kwake hakutaka kabisa kusikia suala
la mume wa mtu au ukewenza. Alitaka ndoa
ya kuimiliki mwenyewe.
Nilitumia Gharama nyingi mpaka kumuweka mikononi. Madalali na
makuadi walizila fedha zangu kwa ajili ya Binti Waseme, kumshawishi asinitoke!.
Mtoto aloumbika. Lugha yake laini. Macho yake makubwa
yaliyopakaliwa wanja mweusi wakati wote. Nywele zake ni gumzo. Sikubahatika
kuziona kwakuwa zilifunikwa na ushungi kila siku.
Miguu wala kiwiko sikuvijua. Zaidi niliambulia kuona kiganja na
Nyayo. Alijistiri katika kila faragha. Hakika nilijivunia kuwa karibu naye,
japo ilikuwa kwa masharti kwamba hakuna mahusiano ya Kimwili mpaka tufunge
ndoa.
Nilishukuru Familia yangu ilikuwa dar. Mke wangu alikuwa na
majukumu mazito ya Kazini kwake. Alikuwa yupo katika ofisi za Umoja wa Mataifa.
Hivyo asingeliweza kupata nafasi ya kuja labda mimi ambaye awali mara kwa mara
nilienda, mwishoni mwa juma.
Watoto wangu wawili walikuwa wanasoma shule za bweni. Hapo Jijini
Dar es salaam. Mmoja la tano na mwingine la tatu. Hivyo Mke wangu
haikumzuia safari zake za kikazi.
Nashukuru hakunilaumu pale ninapopitiliza hadi miezi mitatu bila
kurudi. Naye pia alitumia muda mwingi kwa safari za kikazi na Semina.
Kwakuwa watoto hawakuwepo nyumbani na mume nilikuwa Tanga kwa
muda. Alikuwa huru.
Kijana Sadi Semhando, alikuwa kikwazo kwangu. Yeye alikuwa na kasi ya kumuoa Waseme kuliko mimi.
Tena cha kuumiza zaidi alihitaji kwenda
kujitokeza nyumbani kwao, wakati mimi nilikuwa nahitaji mahusiano tu.
Hapo binti hakusita kunipa msimamo wake ulionachanganya .Alinipigia
simu iliyonifanya niishiwe na nguvu kabisa!.
“Sam. Nisikilize kwa makini. Huu ndiyo msimamo wangu!. Mimi ni
msichana ninayejitambua!. Kama upo tayari na unanihitaji, nakupa wiki moja
kwenda kutoa posa nyumbani. Baada ya wiki usinitafute, tayari nitakubali posa
ya mtu mwingine aliyoileta.
Sina jinsi ya kuwakatalia
Wazazi wangu kwani umri wangu unahitaji niwe na milki katika maisha yangu ya ndoa.Raha
ya mwanamke kumiliki nyumba eeh!. Usipofanya hima nitajua haupo tayari, Wataka
kuharibu maisha yangu tu!.Asante” Waseme alitoa maneno hayo na kukata simu.
Kila nilipopiga haikupokelewa, nilizidi kuchanganyikiwa na
kumpigia dalali mmoja aliyeniunganisha na Waseme. Dalali alikuja haraka kwani
aliona dili yake imechemka.
Dalali: Sasa kwanini unasita kumuoa?
Miye: tatizo nina mke!
Dalali: He kumbe unataka mchepuko! Sasa!oa awe mke wa pili
Sam: Siyo rahisi!. Nilichohitaji ni penzi lake kwa gharama yeyote
ile!. Nisaidie nitakulipa! . Tena nimebakisha miezi miwili, narudi kuendelea na
kazi makao Makuu Dar es salaam.
Dalali: sasa!
Sam: nisaidie nifanyeje!
Dalali: Hapa cha kukusaidia twende kwa babu akaweke mambo
sawa!kisha unaenda mpaka kwao unatangaza ndoa baada ya kumaliza hitaji lako
unakaa naye mwezi unamuacha na kurudi
kwa familia yako!.
Sam: Kwa babu yako?
Dalali: Utamuona!Wazee wa kuweka mambo sawa!
Sam: Poa!, lakini angalia wasije wakaniroga bure?. Hii Tanga line!
Dalali: Sisi ndiyo wa sajili wa line hizo. Ondoa shaka.
Sam:una huhakika!
Dalali: Ndiyo maana nakwambia twende kwa babu wasikushushie mshipa
bure.
Sam: Da hiyo safi haya Twende.Maji ya hiliki, Asmini Kitandani.
Udi na nyimbo ya taarabu inanimaliza ndugu yangu!.
Dalali: Utayajulia wapi mtu wa bara weye. Haya twende!
Mambo yalikuwa mepesi tulienda kwa mzee aliyejulikana kwa jina la
Mara Moja. Alisema hilo jambo kwake analimaliza mara moja kama jina lake la
utani. Sikujua jina lake halisi nani. Tulimueleza utapeli wote. Japo alisita,
lakini fedha ni sabuni ya roho alikubali.
Alikuwa na kilinge chake cha
uganga katikati ya mji , japo yeye mwenyewe nyumba yake ilikuwa mbali na hapo.
Hatimaye dalali alikuwa ndiyo mshenga wangu wa kutoa Posa. Waseme
alifurahi kwa uamuzi wangu wa busara. Muda si mrefu. Mshenga alinitafutia watu
wazima kwa ajili ya kwenda kupeleka mahari. Ikiwa kama ndiyo ndugu zangu wa
bandia.
Kwa bahati mbaya baba yake Mzazi alikuwa amesafiri. Hivyo baba
yake mkubwa alipokea mahari kwa niaba ya ndugu yake.Baba yake Mzazi alitoa
ahadi angelikuwepo siku ya Ndoa.
Ilikuwa siri kubwa pale kazini. Sikutaka mtu yeyote afahamu.
Waseme alikubaliana na wazo langu hilo. Kwani naye pia kuna vijana
wengi walimuhitaji aliwakataa kwa ajili yangu, akiwemo Sadi.
Siku ya Ndoa ilifika. Nilivaa Kanzu vizuri pamoja na Mpambe wangu
ambaye ndiye huyo dalali wangu.
Tulikodi gari hadi Chumbageni ambapo ndipo Wazazi wa Waseme
walipokuwa wakiishi.
Tanga kunako shughuli lol!. Ngoma zilipigwa , tulikuta wanawake
wamevaa sare. Niliambiwa ninatakiwa kuoshwa kwa maji ya hiliki na marashi miguuni
na pia kupakaliwa miski na mafuta ya nazi yaliyotiwa Asmini.
Hapo chakula maalum cha Solo kilikuwa kimeandaliwa kabisa. Dalali
wangu alikuwa anafurahia hilo solo. Nami nilihitaji nilione. Japo nilikuwa
nimejawa na hofu kweli.
Hatimaye tukikaribishwa na
ngoma. Nikiwa na mpambe wangu pamoja na ndugu zangu wa bandia. Tulikaa katika
mkeka. Watoto wa Chuo walikuwa tayari wamesha kaa katika mkeka kwa ajili ya
kaswida.
Umati uliokuwepo pale si wa kawaida. Maturubai matatu yaliwekwa
uwanjani. Inaonyesha wazi wazazi walifurahia sana ndoa ya binti yao. Kwa mbali
niliona majungu ya Shaba yakiwa yamefunikiwa na moto. Harufu ya pilau ilisikika
mtaa mzima.
Moto uliletwa katika chetezo na tayari, ubani ulikuwa ktk
kisahani. Maji ya marashi yakiwa pembeni. Moyo ulikuwa hautaki kutulia.
Nikifikiria dhambi nayoifanya kisa ni kutaka utafiti wa mabinti warembo wa
Tanga.
Hatimaye Baba yake Waseme alikuwa ndani akiweka mambo sawa. Alitoka
akiwa amevaa Kanzu nadhifu, Koti na Kofia.
Sikusubiri akaribie. Niliinamisha kichwa chini ili asinione Bwana harusi
mapepe. Bila kukawia Shekh alikuwa tayari anataka kufungisha ndoa .
Nilinyanyua uso juu kumpa mkono Baba mkwe kwa ajili ya kufungisha
ndoa. Lo! Sote tulitazamana kila mmoja macho yakiwa yamemtoka. Nilihisi kiuno
hakifanyi kazi, huku haja kubwa na ndogo inakosa ufunguo.
Niligeuka kumuangalia mshenga wangu na ndugu wa bandia. Tayari walikuwa
wametoweka. Nilihisi mapigo ya moyo yakishuka
taratibu. Mganga mara moja!, kumbe ndiyo
Baba yake Waseme?. Niliishiwa nguvu. Nikahisi kizuguzungu sikupata tena
fahamu!.
Sehemu ya
Pili
Nilipata fahamu nikiwa hospital ya rufaa Muhimbili jijini Dare s salaam.Tena katika Chumba cha
watu wenye uangalizi maalum. Sikujua walitumia muda gani kunifikisha pale.
Lakini nilisikia wakisema ni siku ya tatu sina fahamu.
Nilipogeuka nilimuona dada yangu akiwa anatoa machozi.Aliponiona
nimefungua macho. Haraka aliwaita madaktari ambao walikuja kuendeleza huduma.
Baada ya muda fahamu zilinijia zaidi. Nilichokumbuka kwa
haraka ni pale nilipomuona Mzee mara
moja na kuanza kujisikia vibaya kwa sababu ya kuumbuka!.
“Kaka nashukuru umerudi tena duniani!” alisema dada yangu huku
akinishika Kichwa.
“Mke wangu anayo habari?” niliuliza. Kwakuwa natambua alikuwa yupo
safari kikazi Arusha.Sikutaka ajue jambo lile.
“Kaka jiangalie afya yako kwa sasa,achana na habari za mke wako!”
alisema Dada yangu.
“Dada anajua jambo hili?” Nilimuuliza tena dada yangu.
“Kaka ngoja upone vizuri. Achana na mambo yajayo angalia afya
yako!” Alisisitiza dada yangu.
Nilijua mke wangu ameshafahamu na sasa katoa maamuzi ya kuachana
na mimi. Nilijutia uasherati wangu wa kutaka michepuko, yamenikuta!. Pia
niliamini dhambi ya kumlaghai binti wa
watu ndiyo iliyopelekea kupata malipo haya.
Hapo sasa naamini ibilisi ya mtu ni mtu. Baada ya Dalali kufanya
yale yote alitoweka kabisa na kuniachia nicheze na fedheha ile. Nilifikiria
Mganga Mara moja ndiyo nimemtendea mwanaye kwa mikono yake, ni hatua gani
atachukua!.Lakini nilikuwa bado sijafika kilele cha mchepuko!.
Hapo nikaamini naye pia atajifunza kutoa huduma za dhambi kama
zile hali akijua sikuwa na nia nzuri juu ya binti niliyetaka kumtendea. Wote
tuliubeba mshahara wa dhambi!
Sijui Waseme atakuwa katika
hali gani!. Msichana aliye na msimamo thabiti, nimemuingiza katika nuksi ya
ndoa na kujikuta ndoa ikiwa haipo tena.
Nakubali kuna wanaume wengine ni wavurugaji kama mimi. Lakini yote
Ibilisi. Ashindindwe na kulegea. Asije tena katika nafsi yangu na kuharibia
watu maisha yao. Namkemea kwa nguvu zote.
Sadi Kijana aliyekuwa tayari kumuoa Waseme. Nimemkatili akabaki
anajutia nafsi yake. Kwani kwangu Rupia ndiyo iliyosaidia kila jambo kuwa
jepesi.
Hata hivyo hali yangu iliimarika na kupelekea kurudi nyumbani.
Dada na shemeji yangu, yaani mume wa dada yangu, waliniambia nitaenda kwao
kwakuwa mke wangu hayupo.
“Shemeji”. Mume wa dada aliniita. “ Mke wako hali yake ilikuwa
mbaya lakini kwa sasa anaendelea vyema naye amelazwa chumba cha pili kwa
uangalizi maalum. Alikuwa njiani kuelekea Arusha, alipopata habari ya kupoteza
kwako fahamu naye hali yake ilibadilika ghafla hakujitambua tena. Haikuwa siri
alijua kila kitu”
alisema Mume wa Dada yangu nilizidi kuchanganyikiwa. Nilitegemea
jambo hilo asingeliweza kulipokea kirahisi. Kufukuzia mchepuko ulinifanya
takribani miezi mitatu sikuwa karibu na mke wangu.
Niliwaomba wanipeleke nikamuangalie. Nilihisi nguvu zinarudi tena.
Japo nilifikiria sana jinsi nitakavyomuangalia usoni. Lakini maji
yalishamwagika hayazoleki.
Tulienda tukamkuta anapewa uji na Mama yake. Huku pembeni walikuwa
ndugu zake wengi, pamoja na baba yake.
Nilipoingia wote waliniangalia kwa jicho la hasira. Sikujali
nilisogea hadi pale alipo mke wangu Desta. Aliponiona alianza kulia. Nilipiga
magoti kumuomba msamaha.
Ndugu zake na wangu walitoka nje na kutuacha. Nilikuwa mwingi wa
soni. Lakini yameshanikuta!. Nayakabili kiume.
“Mume wangu ni kipi ulichokikosa kwangu hadi kunidhalilisha kiasi
hiki. Tena ulitaka kuoa kabisa!. Sasa
unanitafutia nini?.
Kwanini uwe tapeli wa mapenzi kiasi hiki?. Nimepewa mkanda mzima
kutoka kwa Kijana anayeitwa Sadi ambaye ulimpokonya mchumba huyo!. Hali ukijua,
ulitaka tu kutimiza nia. Unamdhalilisha mwanamke, Unachepuka katika ndoa yako,
sasa tizama aibu iliyopo mbele yako!.
Miezi kadhaa hukuhitaji ukaribu nami.Eti kisingizio cha kazi.
Pamoja na majukumu yangu lakini bado nilihitaji nafasi ya kukaa na mume wangu.
Kumbuka Mwanamke bila mwenza hajakamilika!. Umenitia majaribuni Sam!.
Niuweke wapi uso wangu?.
Alisema Mke wangu huku machozi yakimtoka nami nikitumia muda huo kumbembeleza
japo haisaidii kwa machungu aliyo nayo.
Mara aliingia Dakitari. Mke wangu alifuta haraka machozi.
Alitusogelea.
“Desta Unalia nini mama!. Hebu acha kilio na tujadili jambo !.
Huyu ni nani yako?’. Daktari aliuliza.
“Mume wangu” Desta alisema.
“Ooh babari !.”
“Nzuri asante kwa kumjali mke wangu” nilisema. Nilitambua dakitari
yule atakuwa si wale walionihudumia wakati nipo pale. Tayari nilikuwa na nguo
za raia. Si za hospitali tena.
“Vyema nimewaona wote wawili. Nina habari kwenu!. Desta!, kupoteza
fahamu kwako pia kulisababishwa na hali
ya ujauzito.
Kutokana na mshituko mkubwa ulioupata. Ukiwa na mimba ya mwezi
mmoja na wiki moja , hali hiyo isingeweza kuhimili kiumbe kichanga kilichopo
tumboni.Nasikitika kuwaeleza ujauzito huo umetoka. Poleni sana.
Lo! Nilishituka. Ni miezi mitatu sijakutana na mke wangu.
Nilipogeuka kumuangalia Desta, tayari
alikuwa amechanganyikiwa baada ya habari
hiyo. Daktari alijuta kuleta ujumbe wake.
Wauguzi waliingia kumsaidia Desta ambaye mapigo ya moyo yalienda
kwa kasi sana…….
************************************************************
Subiri
sehemu ya tatu na ya mwisho je! Baada ya habari hizo Sam atachukua maamuzi
gani?. Je nani aliyempa ujauzito Desta?. Nani wa kulaumiwa katika hili!...Usikose
uhondo wa mwisho.
Mtunzi-Aunt
Rahma Mahmoud
e-mail: rahmamahmoudmk@yahoo.com