Safari yangu ya Utalii wa ndani
Kaole- Bagamoyo, Pwani
Bagamoyo ni Wilaya iliyopo ndani ya mkoa wa Pwani, Nchini Tanzania, Afrika
Mashariki.
Wilaya hii inasifika kwa historia ya Mambo ya Kale ikiwemo vivutio
vya kitalii. Wakoloni walikuwa wakifanya biashara ya
watumwa.
Jina la Bagamoyo katika historia yake halisi ilikuwa ni Bwagamoyo .
Lakini Baada ya Mzungu kushindwa kutamka, Aliita Bagamoyo. Jina likakua hadi
leo.
Ni eneo lililopendwa na
wafanyabiasha wa utumwa hapo kale, kama kituo chao cha mapumziko na kubwaga
moyo.
Moja ya kivutio nilichokuwa
nakitamani kuona baada ya kupata historia yake ni eneo la
Kaole lenye historia ya kusisimua.
Nikiwa mwana habari na mwandishi wa Vitabu, sikupenda hata kidogo
kupita bila kuhabarisha na kubaki kumbukumbu katika kitabu. Nilihitaji
nishuhudie kwa macho yangu eneo hilo na kulifanyia kazi ndani ya nakala zangu.
Kwa bahati nzuri nilipata likizo fupi ya Sikukuu, hapo ndipo nami
nilipotumia nafasi hiyo nikiwa na familia yangu kudhuru eneo la Kaole.
Haikuwa mwendo mrefu kutoka Dar es salaam mpaka Bagamoyo. Hatimaye nilifika kaole na kujionea maajabu ya vitu vya kale na historia yake.
Ufikapo unakaribishwa kwa
bakshasha na waongozaji wa eneo hilo la kihistoria. utapelekwa sehemu maalumu
ya wageni,yenye viti vilivyopo chini ya mti.
Utaelezwa historia ya Kaole ikifuatiwa na kuelekea sehemu moja
baada ya nyingine kwa ajili ya kujionea maajabu ya mambo ya kale.
Kuna vitu vingi vya kushangaza ikiwemo majengo ya kale, msikiti
uliojengwa kwa mawe, Vyombo mbalimbali vilivyokuwa vikitumika zamani.
Nilivutiwa zaidi na historia ya Kaburi la wapendanao. Kaburi hili
lilikuwa la mke na mume ambao walikuwa Wanapendana sana. Pia wakishirikiana
katika biashara.
Wakati walipokuwa katika harakati za safari ya kibiashara chombo
chao kilizama. Historia yao inasema
kutokana na mapenzi ya dhati waliyonayo, waliamua kujifunga nguo pamoja ili
kama kufa wafe pamoja. Wakafariki wote wakiwa wamejifunga nguo hiyo.
Watu waliopoa miili yao ikiwa imejifunga pamoja. Kwa heshima
waliamua kuwazika pamoja kama ambavyo waliona walivyojifunga. Japo Kaburi
lilikuwa moja lakini kila mmoja alizikwa mwanadani wake.
Kufuatia historia ile tangu wakati ule mpaka leo, mume na mke au wachumba, wamekuwa wakienda pale kujiapiza katika ndoa au mapenzi yao yasivurugike. Awe Mwafrika, Mzungu n,k wamekuwa na imani ya kupata mapenzi ya dhati wajiapizapo katika kaburi la wapendanao
Maji ya ajabu
Kuna kisima ambacho kimekuwa ni kivutio. tangu karne na karne lakini hakijawahi kukauka.
Hakina maji mengi, Ila unaweza ukachota ujaze mapipa uwezavyo, bado maji yale yasihisi kupungua.
Si mengi ukiyaona wala kisima si kirefu, lakini hayaishi.
Ajabu ya maji yale yapo karibu na bahari ila yenyewe ni baridi
hayana chumvi hata kidogo. Unaweza kunywa na kufanyia utakacho.
Maji hayo yamekuwa yakiheshimiwa na kutukuzwa sana.Wakiamini ni
maji ya baraka. Wengi huenda kwa ajili
ya kuyachota ili kuyaoga waondoe matatizo yao.
Kaburi la Msichana mtabiri
Katika historia yake kulikuwa na msichana mdogo, alikuwa mtabiri
wa mambo mbalimbali. Watu walikuwa wakitabiriwa mambo yajayo ambayo walikuwa
wakiyaona baada ya utabiri huo.
Utabiri wake ukampa umaarufu katika umri mdogo. Akiwa na Umri wa
miaka 14 alifariki ghafla, ikafuatiwa na watoto wengine kufariki ghafla katika
siku aliyofariki binti huyo. Kutokana na imani waliyonayo, walimzika yule binti
na pembeni yake waliwazika Wale watoto
watatu wakiamini ni malaika.
Sehemu hiyo, pia watu wamekuwa wakienda kuomba ili kuondokewa na matatizo mbalimbali.
Mbuyu wa ajabu
Mbuyu huu unaambiwa kuna upande mmoja ukizunguka unaongeza siku za
kuishi na upande mwingine ukizunguka, unapunguza siku za kuishi. Wengi wamekuwa
wakienda pale tangu enzi za kale ili kuzunguka.
Kitu kingine katika mbuyu huu umekuwa ukigongwa misumari mingi na watu toka enzi za zamani mpaka leo. Huamini wanapoigongelea misumari katika mbuyu ule husamehewa dhambi zao. Mbuyu huo una miaka mingi sana na misumari mingine imekuwa tayari imeanza kufunikwa na magome.
Bandari ya kale
Upande wa chini katika eneo hilo la Kaole kulikuwa na kivutio cha bandari
kuu hapo kale. Lakini haikuendelezwa ili
kuikuza historia hiyo. Mikoko bado inaonekana kuwepo. Kwa sasa maji yakipwa na
kujaa huingia eneo hilo japo si mengi kama awali.
Bagamoyo kuna mambo mengi ya kuvutia. Njia zake za zamani,huwa ni
kivutio. Maeneo mengi hufanana na yale ya visiwani Zanzibar.
Livingstone hotel
Kaole
Bagamoyo-Pwani
Tanzania
East-Africa
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni