Aunt Rahma Shopping Centre

Aunt Rahma Shopping Centre
Kariakoo/Tabata Muuzaji wa nguo mbalimbali za watoto na wakubwa kwa bei poa kutoka China na Dubai

Ijumaa, 16 Oktoba 2015

Riwaya


Msomaji wa Blog  yangu ya Auntrahmaonlinetz, nilitoa sehemu ya kwanza ya riwaya na kuiacha kwa muda kutokana na majukumu. Sasa nairejesha na kuunganisha sehemu ya pili ya hadithi Safari ya Tanga. Ni riwaya yenye kuburudisha na kuelimisha

 Safari ya Tanga
Nimepewa barua ya kikazi kwenda mkoani Tanga kwa muda wa miezi sita, baada meneja aliyekuwepo  hapo, kupata matatizo ya Kiafya. Mji ulikuwa mgeni kwangu. Familia yangu, ikiwemo mke na watoto niliwaacha jijini Dar es salaam.
Mke wangu hakusita kuniusia juu ya jiji la Tanga lenye Wanawake warembo na lugha laini. Alinionya sana mchepuko wa Tanga siyo dili. Ukijaribu unazama moja kwa moja na kusahau familia yako.
Alinieleza maji ya kuoga utawekewa hiliki na asmini kitandani hapo unaweza kujisahau.Utaimbiwa taarabu nyepesi za Bi Shakira na kuingia mtegoni.Huku udi ukinukia chumba kizima mbali na mwanandani mwenyewe, aliyejiosha kwa maji ya Waridi.
Niliapa  nitaenda kwa kile kilichonipeleka na si kingine.Nilifuata moja huko, sikubali kumi na moja. Mtoto wa bara miye mambo hayo kwangu siyo!.
Mh!. Kuanzia kazini mpaka nyumbani ilikuwa mitego mitupu. Hatimaye nikajikuta pendo linazama kwa binti aliyekuwa katibu muhktasi wetu pale ofisini. Haikuwa kazi rahisi kumpata kama nilivyoelezwa.
Mtoto wa Kisegeju alikuwa hategeki. Alijiwekea msimamo thabiti. Hapo nikaamini kwamba si Wanawake wa kitanga wepesi kila mwanadamu na hulka yake.
Alinichanganya vilivyo mtoto Waseme. Aingiapo kazini, utasikia harufu nzuri ya uturi kuanzia mlangoni. Hapo akili zote zilihama. Usia wa mama watoto nikatupia kule!.
Binti huyu Waseme alinitoa jasho!.Ilinibidi nitumie nguvu za ziada  kuwa karibu na mimi.
Tayari alishaingia katika kumi na nane zangu. Nilimficha kwamba sijaoa. Binti wa kitanga niliapa kutomkosa. Kwake hakutaka kabisa kusikia suala  la mume wa mtu au ukewenza. Alitaka ndoa ya kuimiliki mwenyewe.
Nilitumia Gharama nyingi mpaka kumuweka mikononi. Madalali na makuadi walizila fedha zangu kwa ajili ya Binti Waseme, kumshawishi asinitoke!.
Mtoto aloumbika. Lugha yake laini. Macho yake makubwa yaliyopakaliwa wanja mweusi wakati wote. Nywele zake ni gumzo. Sikubahatika kuziona kwakuwa zilifunikwa na ushungi kila siku.
Miguu wala kiwiko sikuvijua. Zaidi niliambulia kuona kiganja na Nyayo. Alijistiri katika kila faragha. Hakika nilijivunia kuwa karibu naye, japo ilikuwa kwa masharti kwamba hakuna mahusiano ya Kimwili mpaka tufunge ndoa.
Nilishukuru Familia yangu ilikuwa dar. Mke wangu alikuwa na majukumu mazito ya Kazini kwake. Alikuwa yupo katika ofisi za Umoja wa Mataifa. Hivyo asingeliweza kupata nafasi ya kuja labda mimi ambaye awali mara kwa mara nilienda, mwishoni mwa juma.
Watoto wangu wawili walikuwa wanasoma shule za bweni. Hapo Jijini Dar es salaam. Mmoja la tano na mwingine la tatu. Hivyo Mke wangu haikumzuia  safari zake za kikazi.
Nashukuru hakunilaumu pale ninapopitiliza hadi miezi mitatu bila kurudi. Naye pia alitumia muda mwingi kwa safari za kikazi na Semina.
Kwakuwa watoto hawakuwepo nyumbani na mume nilikuwa Tanga kwa muda. Alikuwa huru.
Kijana Sadi Semhando, alikuwa kikwazo kwangu. Yeye alikuwa na kasi ya kumuoa Waseme kuliko mimi. Tena cha kuumiza zaidi  alihitaji kwenda kujitokeza nyumbani kwao, wakati mimi nilikuwa nahitaji mahusiano tu.
Hapo binti hakusita kunipa msimamo wake ulionachanganya .Alinipigia simu iliyonifanya niishiwe na nguvu kabisa!.
“Sam. Nisikilize kwa makini. Huu ndiyo msimamo wangu!. Mimi ni msichana ninayejitambua!. Kama upo tayari na unanihitaji, nakupa wiki moja kwenda kutoa posa nyumbani. Baada ya wiki usinitafute, tayari nitakubali posa ya mtu mwingine aliyoileta.
 Sina jinsi ya kuwakatalia Wazazi wangu kwani umri wangu unahitaji niwe na milki katika maisha yangu ya ndoa.Raha ya mwanamke kumiliki nyumba eeh!. Usipofanya hima nitajua haupo tayari, Wataka kuharibu maisha yangu tu!.Asante” Waseme alitoa maneno hayo na kukata simu.
Kila nilipopiga haikupokelewa, nilizidi kuchanganyikiwa na kumpigia dalali mmoja aliyeniunganisha na Waseme. Dalali alikuja haraka kwani aliona dili yake imechemka.
Dalali: Sasa kwanini unasita kumuoa?
Miye: tatizo nina mke!
Dalali: He kumbe unataka mchepuko! Sasa!oa awe mke wa pili
Sam: Siyo rahisi!. Nilichohitaji ni penzi lake kwa gharama yeyote ile!. Nisaidie nitakulipa! . Tena nimebakisha miezi miwili, narudi kuendelea na kazi makao Makuu Dar es salaam.
Dalali: sasa!
Sam: nisaidie nifanyeje!
Dalali: Hapa cha kukusaidia twende kwa babu akaweke mambo sawa!kisha unaenda mpaka kwao unatangaza ndoa baada ya kumaliza hitaji lako unakaa naye mwezi unamuacha  na kurudi kwa familia yako!.
Sam: Kwa babu yako?
Dalali: Utamuona!Wazee wa kuweka mambo sawa!
Sam: Poa!, lakini angalia wasije wakaniroga bure?. Hii Tanga line!
Dalali: Sisi ndiyo wa sajili wa line hizo. Ondoa shaka.
Sam:una huhakika!
Dalali: Ndiyo maana nakwambia twende kwa babu wasikushushie mshipa bure.
Sam: Da hiyo safi haya Twende.Maji ya hiliki, Asmini Kitandani. Udi na nyimbo ya taarabu inanimaliza ndugu yangu!.
Dalali: Utayajulia wapi mtu wa bara weye. Haya twende!
Mambo yalikuwa mepesi tulienda kwa mzee aliyejulikana kwa jina la Mara Moja. Alisema hilo jambo kwake analimaliza mara moja kama jina lake la utani. Sikujua jina lake halisi nani. Tulimueleza utapeli wote. Japo alisita, lakini fedha ni sabuni ya roho alikubali.
 Alikuwa na kilinge chake cha uganga katikati ya mji , japo yeye mwenyewe nyumba yake ilikuwa mbali na hapo.
Hatimaye dalali alikuwa ndiyo mshenga wangu wa kutoa Posa. Waseme alifurahi kwa uamuzi wangu wa busara. Muda si mrefu. Mshenga alinitafutia watu wazima kwa ajili ya kwenda kupeleka mahari. Ikiwa kama ndiyo ndugu zangu wa bandia.
Kwa bahati mbaya baba yake Mzazi alikuwa amesafiri. Hivyo baba yake mkubwa alipokea mahari kwa niaba ya ndugu yake.Baba yake Mzazi alitoa ahadi angelikuwepo siku ya Ndoa.
Ilikuwa siri kubwa pale kazini. Sikutaka mtu yeyote afahamu.
Waseme alikubaliana na wazo langu hilo. Kwani naye pia kuna vijana wengi walimuhitaji aliwakataa kwa ajili yangu, akiwemo Sadi.
Siku ya Ndoa ilifika. Nilivaa Kanzu vizuri pamoja na Mpambe wangu ambaye ndiye huyo dalali wangu.
Tulikodi gari hadi Chumbageni ambapo ndipo Wazazi wa Waseme walipokuwa wakiishi.
Tanga kunako shughuli lol!. Ngoma zilipigwa , tulikuta wanawake wamevaa sare. Niliambiwa ninatakiwa kuoshwa kwa maji ya hiliki na marashi miguuni na pia kupakaliwa miski na mafuta ya nazi yaliyotiwa Asmini.
Hapo chakula maalum cha Solo kilikuwa kimeandaliwa kabisa. Dalali wangu alikuwa anafurahia hilo solo. Nami nilihitaji nilione. Japo nilikuwa nimejawa na hofu kweli.
Hatimaye  tukikaribishwa na ngoma. Nikiwa na mpambe wangu pamoja na ndugu zangu wa bandia. Tulikaa katika mkeka. Watoto wa Chuo walikuwa tayari wamesha kaa katika mkeka kwa ajili ya kaswida.
Umati uliokuwepo pale si wa kawaida. Maturubai matatu yaliwekwa uwanjani. Inaonyesha wazi wazazi walifurahia sana ndoa ya binti yao. Kwa mbali niliona majungu ya Shaba yakiwa yamefunikiwa na moto. Harufu ya pilau ilisikika mtaa mzima.
Moto uliletwa katika chetezo na tayari, ubani ulikuwa ktk kisahani. Maji ya marashi yakiwa pembeni. Moyo ulikuwa hautaki kutulia. Nikifikiria dhambi nayoifanya kisa ni kutaka utafiti wa mabinti warembo wa Tanga.
Hatimaye Baba yake Waseme alikuwa ndani akiweka mambo sawa. Alitoka akiwa amevaa Kanzu nadhifu, Koti na Kofia.  Sikusubiri akaribie. Niliinamisha kichwa chini ili asinione Bwana harusi mapepe. Bila kukawia Shekh alikuwa tayari anataka kufungisha ndoa .
Nilinyanyua uso juu kumpa mkono Baba mkwe kwa ajili ya kufungisha ndoa. Lo! Sote tulitazamana kila mmoja macho yakiwa yamemtoka. Nilihisi kiuno hakifanyi kazi, huku haja kubwa na ndogo inakosa ufunguo.
Niligeuka kumuangalia mshenga wangu na ndugu wa bandia. Tayari walikuwa  wametoweka. Nilihisi mapigo ya moyo yakishuka taratibu. Mganga mara moja!,  kumbe ndiyo Baba yake Waseme?. Niliishiwa nguvu. Nikahisi kizuguzungu sikupata tena fahamu!.
Sehemu ya Pili
Nilipata fahamu nikiwa hospital ya rufaa Muhimbili  jijini Dare s salaam.Tena katika Chumba cha watu wenye uangalizi maalum. Sikujua walitumia muda gani kunifikisha pale. Lakini nilisikia wakisema ni siku ya tatu sina fahamu.
Nilipogeuka nilimuona dada yangu akiwa anatoa machozi.Aliponiona nimefungua macho. Haraka aliwaita madaktari ambao walikuja  kuendeleza huduma.
Baada ya muda fahamu zilinijia zaidi. Nilichokumbuka kwa haraka  ni pale nilipomuona Mzee mara moja na kuanza kujisikia vibaya kwa sababu ya kuumbuka!.
“Kaka nashukuru umerudi tena duniani!” alisema dada yangu huku akinishika Kichwa.
“Mke wangu anayo habari?” niliuliza. Kwakuwa natambua alikuwa yupo safari kikazi Arusha.Sikutaka ajue jambo lile.
“Kaka jiangalie afya yako kwa sasa,achana na habari za mke wako!” alisema Dada yangu.
“Dada anajua jambo hili?” Nilimuuliza tena dada yangu.
“Kaka ngoja upone vizuri. Achana na mambo yajayo angalia afya yako!” Alisisitiza dada yangu.
Nilijua mke wangu ameshafahamu na sasa katoa maamuzi ya kuachana na mimi. Nilijutia uasherati wangu wa kutaka michepuko, yamenikuta!. Pia niliamini dhambi  ya kumlaghai binti wa watu ndiyo iliyopelekea kupata malipo haya.
Hapo sasa naamini ibilisi ya mtu ni mtu. Baada ya Dalali kufanya yale yote alitoweka kabisa na kuniachia nicheze na fedheha ile. Nilifikiria Mganga Mara moja ndiyo nimemtendea mwanaye kwa mikono yake, ni hatua gani atachukua!.Lakini nilikuwa bado sijafika kilele cha mchepuko!.
Hapo nikaamini naye pia atajifunza kutoa huduma za dhambi kama zile hali akijua sikuwa na nia nzuri juu ya binti niliyetaka kumtendea. Wote tuliubeba mshahara wa dhambi!
Sijui  Waseme atakuwa katika hali gani!. Msichana aliye na msimamo thabiti, nimemuingiza katika nuksi ya ndoa na kujikuta ndoa ikiwa haipo tena.
Nakubali kuna wanaume wengine ni wavurugaji kama mimi. Lakini yote Ibilisi. Ashindindwe na kulegea. Asije tena katika nafsi yangu na kuharibia watu maisha yao. Namkemea kwa nguvu zote.
Sadi Kijana aliyekuwa tayari kumuoa Waseme. Nimemkatili akabaki anajutia nafsi yake. Kwani kwangu Rupia ndiyo iliyosaidia kila jambo kuwa jepesi.
Hata hivyo hali yangu iliimarika na kupelekea kurudi nyumbani. Dada na shemeji yangu, yaani mume wa dada yangu, waliniambia nitaenda kwao kwakuwa mke wangu hayupo.
“Shemeji”. Mume wa dada aliniita. “ Mke wako hali yake ilikuwa mbaya lakini kwa sasa anaendelea vyema naye amelazwa chumba cha pili kwa uangalizi maalum. Alikuwa njiani kuelekea Arusha, alipopata habari ya kupoteza kwako fahamu naye hali yake ilibadilika ghafla hakujitambua tena. Haikuwa siri alijua kila kitu”
alisema Mume wa Dada yangu nilizidi kuchanganyikiwa. Nilitegemea jambo hilo asingeliweza kulipokea kirahisi. Kufukuzia mchepuko ulinifanya takribani miezi mitatu sikuwa karibu na mke wangu. 
Niliwaomba wanipeleke nikamuangalie. Nilihisi nguvu zinarudi tena. Japo nilifikiria sana jinsi nitakavyomuangalia usoni. Lakini maji yalishamwagika hayazoleki.
Tulienda tukamkuta anapewa uji na Mama yake. Huku pembeni walikuwa ndugu zake wengi, pamoja na baba yake.
Nilipoingia wote waliniangalia kwa jicho la hasira. Sikujali nilisogea hadi pale alipo mke wangu Desta. Aliponiona alianza kulia. Nilipiga magoti kumuomba msamaha.
Ndugu zake na wangu walitoka nje na kutuacha. Nilikuwa mwingi wa soni. Lakini yameshanikuta!. Nayakabili kiume.
“Mume wangu ni kipi ulichokikosa kwangu hadi kunidhalilisha kiasi hiki. Tena ulitaka kuoa  kabisa!. Sasa unanitafutia nini?.
Kwanini uwe tapeli wa mapenzi kiasi hiki?. Nimepewa mkanda mzima kutoka kwa Kijana anayeitwa Sadi ambaye ulimpokonya mchumba huyo!. Hali ukijua, ulitaka tu kutimiza nia. Unamdhalilisha mwanamke, Unachepuka katika ndoa yako, sasa tizama aibu iliyopo mbele yako!.
Miezi kadhaa hukuhitaji ukaribu nami.Eti kisingizio cha kazi. Pamoja na majukumu yangu lakini bado nilihitaji nafasi ya kukaa na mume wangu. Kumbuka Mwanamke bila mwenza hajakamilika!. Umenitia majaribuni Sam!.
Niuweke  wapi uso wangu?. Alisema Mke wangu huku machozi yakimtoka nami nikitumia muda huo kumbembeleza japo haisaidii kwa machungu aliyo nayo.
Mara aliingia Dakitari. Mke wangu alifuta haraka machozi. Alitusogelea.
“Desta Unalia nini mama!. Hebu acha kilio na tujadili jambo !. Huyu ni nani yako?’. Daktari aliuliza.
“Mume wangu” Desta alisema.
“Ooh babari !.”
“Nzuri asante kwa kumjali mke wangu” nilisema. Nilitambua dakitari yule atakuwa si wale walionihudumia wakati nipo pale. Tayari nilikuwa na nguo za raia. Si za hospitali tena.
“Vyema nimewaona wote wawili. Nina habari kwenu!. Desta!, kupoteza fahamu kwako pia kulisababishwa na hali  ya ujauzito.
Kutokana na mshituko mkubwa ulioupata. Ukiwa na mimba ya mwezi mmoja na wiki moja , hali hiyo isingeweza kuhimili kiumbe kichanga kilichopo tumboni.Nasikitika kuwaeleza ujauzito huo umetoka. Poleni sana.
Lo! Nilishituka. Ni miezi mitatu sijakutana na mke wangu. Nilipogeuka kumuangalia  Desta, tayari alikuwa amechanganyikiwa  baada ya habari hiyo. Daktari alijuta kuleta ujumbe wake.
Wauguzi waliingia kumsaidia Desta ambaye mapigo ya moyo yalienda kwa kasi sana…….
************************************************************
Subiri sehemu ya tatu na ya mwisho je! Baada ya habari hizo Sam atachukua maamuzi gani?. Je nani aliyempa ujauzito Desta?. Nani wa kulaumiwa katika hili!...Usikose uhondo wa mwisho.
Mtunzi-Aunt Rahma Mahmoud

Maoni 1 :


  1. Salaam!
    Inbox
    Mohamed O. Lupinga

    10:51 (7 minutes ago)


    to rahmamahmoudmk
    Salaam tele Aunti Rahma Mahmoud!

    Mimi ni mwandishi wa kujitolea wa Wikipedia ya Kiswahili, pia ni mwandishi wa riwaya. Hadi sasa nimeandika riwaya 10 huku nikiandika makala 15,000 katika Wikipedia ya Kiswahili.

    Nimepata kusoma riwaya zako kadhaa mpaka sasa.

    1. Kisiwa cha Kuzimu
    2. Yule binti anayeteswa na mama wa kufikia kwa kutupa funguo, akaipata ndani ya samaki.
    3. Kuhusu kijana asiyejua kusoma akapeleka barua kwa kusema maneno ya uwongo baada ya kusomewa ndivyo sivyo na kijana mwenzake.

    Kifupi nimefurahia sana hadithi zako.

    Ningependa nikuandike katika Wikipedia ya Kiswahili japo kuna mtu alijaribu nimeona!

    Namba yangu ya simu ni 0713538427 / 0787232580

    Wako,

    Muddyb.

    Mail Delivery Subsystem

    10:52 (7 minutes ago)


    to me

    Translate message
    Turn off for: English
    Error Icon
    Address not found
    Your message wasn't delivered to rahmamahmoudmk@yahoo.com because the address couldn't be found or is unable to receive email.
    The response from the remote server was:

    554 30 Sorry, your message to rahmamahmoudmk@yahoo.com cannot be delivered. This mailbox is disabled (554.30).



    JibuFuta